MLM Gateway - Helping network marketers build their business

Palamagamba Kabudi: Maswali utetezi wa Tanzania kuhusu kutoshiriki mkutano wa EAC


Waziri wa mambo ya nje wa Tanzania amezua mjadala baada ya kudai kwamba mkutano uliofanyika wiki hii kuzungumzia janga la virusi vya corona haukuwa mkutano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Prof Palamagamba Kabudi alisema mkutano huo uliowahusisha viongozi wa Kenya, Uganda, Rwanda na Sudan Kusini ulikuwa mkutano wa Ushoroba wa Kaskazini.

Tamko lake limezua maswali mengi; je, mkutano huo ulikuwa wa aina gani hasa na nini maana yake?

Tanzania ilikuwa na taarifa?

Prof Kabudi anasema Tanzania iliarifiwa kuhusu mkutano huo uliofanyika kwa njia ya video, lakini anaonekana kudokeza kwamba haikualikwa.

"Ushoroba wa Kaskazini wakikutana wanatuarifu, lakini kwa nini tuhudhurie mkutano wa Ushoroba wa Kaskazini? Ni wa kwao. Ule haukuwa mkutano wa EAC," alisema waziri huyo bungeni.

Alisema kutolewa kwa taarifa kunatokana na mzozo uliotokea mwaka 2013 hadi Jakaya Kikwete akafika bungeni kutoa hotuba kuhusu Jumuiya ya Afrika Mashariki. Waziri alidokeza kwamba kabla ya hapo, mikutano ilikuwa ikifanyika bila Tanzania kufahamishwa.

Tusiruhusu maadui zetu kutaka kuitingisha Jumuiya ya Afrika Mashariki. Wana yao, na sisi tusiwe sehemu ya hayo. Ndwele si sifa lakini Tanzania haijawahi kuacha kusimamia maslahi yake," alisema.

Alisisitiza kwamba mkutano huo ulikuwa wa mashauriano wa viongozi wa mataifa ya Ushoroba wa Kaskazini, na aliarifiwa na waziri wa mambo ya nje wa Rwanda.

Madai yake kuhusu ngazi ya mkutano huo hata hivyo yanakinzana na taarifa zilizotolewa kuhusu mkutano huo.

Taarifa ya tamko la pamoja iliyotolewa na sektretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki baada ya mkutano huo inaueleza kama mkutano wa mashauriano wa viongozi wa mataifa ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Tamko hilo lina nembo za EAC na pia linaeleza kuwa viongozi hao walipokea ripoti ya mkutano wa mawaziri wa jumuiya kuhusu juhudi na hatua zinazochukuliwa kukabiliana na virusi vya corona.

Viongozi hao walizungumzia umuhimu wa kubadilishana habari kipindi hiki cha mlipuko wa ugonjwa huo na pia suala la kuwafuatilia madereva wa masafa marefu.


Bendera za nchi wanachama wa Jumuia ya Afrika Mashariki
Bendera za nchi wanachama wa Jumuia ya Afrika Mashariki

Suala hilo la madereva limekuwa sugu baada ya visa vingi kuripotiwa miongoni mwao. Kenya na Uganda zimeweka masharti mipakani kwa madereva kupimwa kabla ya kuruhusiwa kuendelea na safari zao.

Msemaji wa serikali ya Tanzania Dkt Hassan Abbasi kwenye mahojiano na kipindi cha Dira ya Dunia cha BBC Swahili alidokeza kwamba taifa hilo lilishiriki mkutano wa mawaziri wa EAC na wataalamu wa afya.

Taarifa ya EAC inaonyesha Tanzania iliwakilishwa na Waziri wa Afya Ummy Mwalimu kwenye mkutano huo wa mawaziri mwezi Aprili.

Lakini kuhusu mkutano wa viongozi wa nchi za EAC, Msemaji wa serikali ya Tanzania, Dkt Abbasi alisema kila mkutano ambao taifa hilo limealikwa au ni mwenyeji limekuwa likishiriki.

Muandaaji wa mkutano huo anaelezwa kwenye barua hiyo ya EAC kuwa ni Rais wa Rwanda Paul Kagame ambaye ni ndiye mwenyekiti wa sasa wa EAC.

Taarifa ya ikulu za Kenya na Uganda pia zinaueleza kama mkutano wa viongozi wa EAC.

Utata unaotokea ni kwamba mataifa yaliyohudhuria ndio pia wanachama wa Ushoroba wa Kaskazini. Hata hivyo, mwandalizi wa mkutano na mawasiliano yametolewa kupitia mkutano sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Je, hii ni ishara ya mgawanyiko kwenye jumuiya hiyo?

Kanda ya video iliyowekwa kwenye akaunti ya YouTube ya Rais Kagame inamuonesha kwenye mkutano huo akisisitiza umuhimu wa mataifa yote wanachama kufanya kazi kwa pamoja.

Hata hivyo, anaeleza kwamba kujivuta kwa mwanachama mmoja au wawili hakufai kuwazuia wengine kuendelea.

''Iwapo sote sita hatuwezi kufanya kazi na kuendeleza mambo, haina maana kwamba wawili, watatu au wanne hawawezi kufanya kazi katika hali hii kukabiliana na changamoto tunazokumbana nazo," alisema.

Rais Uhuru Kenyatta pia alihimiza umuhimu wa umoja katika kanda katika kukabiliana na janga la Covid-19.




Rais wa Tanzania, Dokta John Magufuli
Rais wa Tanzania, Dk. John Magufuli

Kukwama kwa mikutano

Mkutano huo wa mashauriano ulifanyika baada ya kukwama kwa mikutano mikuu ya viongozi wa nchi wanachama wa EAC mara ya tatu.

Karibuni zaidi, mkutano usio wa kawaida uliopangiwa kujadili janga la corona ulifaa kufanyika 15 Aprili kwa njia ya video lakini ukaahirishwa kutokana na ombi la Rais wa Sudan Kusini.

Mkutano mkuu wa kawaida pia uliahirishwa Februari kutokana na ombi la Sudan Kusini, ambayo ilisema kuundwa kwa Serikali ya mseto kungeathiri mpangilio na shughuli za kiserikali.

Mkutano huo ulikuwa awali umepangiwa kufanyika 30 Novemba 2019 lakini ukaahirishwa baada ya mmoja wa taifa wanachama kusema hangeweza kushiriki.

Ilitokeaje wakati wa Rais Kikwete?

Waziri wa mambo ya nje wa Tanzania Profesa Kabudi alizungumzia yaliyotokea enzi za Rais Kikwete, Ni kipindi ambapo uhusiano baina ya nchi wanachama wa EAC ulikuwa umedorora sana.

Mapema mwaka huo, Bw Kikwete alikuwa ameziomba Rwanda na Uganda kufanya mazungumzo na waasi waliokuwa wakiendesha vita dhidi ya mataifa hayo kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Tanzania baadaye ilituma wanajeshi wake chini ya mwavuli wa Umoja wa Mataifa kukabiliana na waasi wa M23 ambao Rwanda na Uganda zilidaiwa kuwaunga mkono ingawa zilikanusha madai hayo.

Kiongozi huyo aliwakosoa viongozi wa Kenya, Rwanda na Uganda kwa kufanya maamuzi yaliyohusu EAC bila kuwashirikisha wanachama wengine katika mikutano mitatu iliyokuwa imeandaliwa Entebbe, Mombasa na Kigali .

Viongozi wa nchi wanachama wa Jumuia ya Afrika Mashariki
Marais wa Afrika mashariki Uhuru Kenyatta, Paul kagame, Yoweri Museveni na John Pombe Magufuli

Mataifa hayo matatu yalikuwa yamefanya mikutano mitatu bila kushirikisha Tanzania na Burundi.

Baadhi ya mambo yaliyojadiliwa katika mikutano hiyo ilikuwa ni pamoja nakujenga reli ya kisasa kutoka Mombasa hadi Kampala, Kigali na Bujumbura; ujenzi wa bomba la mafuta la kutoka Kenya hadi Uganda na Sudani ya Kusini na kujengwa kwa kiwanda cha kusafisha mafuta nchini Uganda. Kulikuwa pia masuala ya himaya ya ushuru na forodha EAC na pia kuharakishwa kwa shirikisho.

"Sababu ya wenzetu watatu kuamua kufanya mambo yahusuyo Jumuiya yetu peke yao kwa kweli haieleweki," alilieleza bunge tarehe 7 Novemba, 2013.

"Tunasikia eti kuwa baadhi yao walipoulizwa kwa nini wengine hatupo wakasema kuwa wao wametangulia na sisi tutakapokuwa tayari tutajiunga. Yaani wana Umoja wa Waliokuwa Tayari (Coalition of the Willing).

"Hivi ni nani hayuko tayari (who is not willing?). Haiwezekani watu waitane wenyewe bila ya kutualika halafu wadai kuwa wao ndiyo wako tayari na kujenga dhana kuwa sisi wasiotualika ndiyo ambao hatuko tayari."

Bw Kikwete alisema kwa maoni yake msimamo wa Tanzania kuhusu kuharakisha Shirikisho na masuala ya ardhi, ajira, uhamiaji ndiyo yaliyokuwa chanzo cha uhasama.


Share:

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

Kumbukumbu la Blogu

MAARUFU

ZA HIVI KARIBUNI