"Nilikuwa namnyonyesha mtoto wangu kisha nikaanza kufikiria wengine na kuhuzunika sana. Niliona vile wale watoto wengine wanavyotaabika," amesema Firooza Omar.
Jumanne wiki hii, watu karibia 24 ikiwemo watoto wachanga, kina mama na wauguzi waliuawa kinyama kufuatia shambulio lililotekelezwa na wanamgambo katika chumba cha kujifungua kina mama nchini Afghanistan mjini Kabul.
Firooza, 27, alisikia kuhusu shambulio hilo kupitia televisheni. Alielewa ukubwa wa tatizo lililopo baada ya kuzungumza na rafiki yake na kuona picha mbaya za shambulio zilizokuwa kwenye mitandao ya kijamii.
Yeye mwenye ni mama wa mtoto mvulana wa miezi minne.

Wakati anamnyonyesha mtoto wake, alijiwa na fikra za watoto wengine walioachwa mayatima.
Utu na ujasiri
Ameamua kwenda kusaidia watoto wengine wachanga waliopoteza mama zao katika shambulio hilo.
Kilichofuata ni kuonesha ukarimu wake na ujasiri alio nao.

"Wakati ulipokuwa unawadiwa wa kufungua baada ya kufunga, (shambulio hilo limetekelezwa wakati wa Ramadhani, mwezi mtukufu wa Kiislamu), nilimwambia mume wangu kuhusu nia yangu ya kusaidia watoto ambao wamekuwa mayatima."
Mume wake alimkubalia moja kwa moja na kumuhakikishia kwamba atakuwa anamuangalia kijana wao nyumbani.
Wakati huo Vikosi Maalum vya Afghan vilinusuru kina mama na watoto 100 katika hospitali ya Dasht-e-Barchi na idadi kubwa ya watoto wachanga wakapelekwa katika hospitali ya watoto ya Ataturk takribani kilomita 2 kutoka pale anapoishi Firooza.
Watoto wakili
Umbali aliotembea kwa gari huenda ulikuwa mfupi zaidi lakini wenye kuhatarisha maisha yake katika mji ulioghadhabishwa, kushtuma na kuingiwa na hofu baada ya kutokea kwa shambulio.

"Nilipokwenda hospitalini, niliona watoto karibia 20. Baadhi yao walikuwa wamejeruhiwa. Nilizungumza na wauguzi na wakaniambia kwamba ninyonyesha watoto wanaolia sana."
Kisha akanyonyesa watoto wanne, mmoja baada ya mwengine.
Kabla ya Firooza kuwasili, wauguzi walikuwa wanajaribu kuwapa chakula kilichotengenezwa kwa maziwa ya unga.
"Baadhi ya watoto walikuwa wanakataa kunywa maziwa hayo." Firooza anakumbuka.
Kutuliza watoto waliokuwa wanalia hospitali
Aliwapa watoto hao matumaini ya kuendelea kuishi.

"Nilipowanyonyesha walitulia. Nilifurahi kuweza kuwasaidia."
Baada ya kurejea nyumbani, ilikuwa ni zamu ya kijana wake kunyonya.
"Baada ya saa mbili, nilimnyonyesha mtoto wangu wa kiume." Firooza anasema.
Aliandika kuhusu tajriba hiyo aliopata kwenye mtandao wa kijamii na kusihi kina mama wengine kwenda kwenye hospitali hiyo kusaidia kunyamazisha watoto wengine waliokuwa wanalia
Anasema baadhi ya wanawake wamejitokeza na kunyonyesha watoto hao.
Baada ya usiku wa shambulio, Firooza pia amefanikiwa kutembela hospitali hiyo siku mbili zilizofuata.
Anasema hilo limewezekana kwasababu mume wake anamuunga mkono na kumsihi kufanya hivyo.
'Uhalifu wa kivita'
Hadi kufikia sasa hakuna ambaye amedai kuhusika na shambulio hilo lililotokea Jumanne, ambalo limeelezewa na makundi ya kutetea Haki za Binadamu kama 'uhalifu wa kivita'.
Serikali ya Kabul imeagiza jeshi kutafuta waliotekeleza shambulio hilo.

Aidha, mji wa Kabul umekuwa ukishuhudia ghasia katika kipindi cha miongo minne iliyopita ya vita na migogoro.
Vifo vilivyotokea wiki hii kwa kina mama na watoto wachanga kutakumbukwa kama moja ya matukio mabaya zaidi kuwahi kutokea duniani.
Firooza anasema amefadhaishwa na ghasia zisizoisha ambazo zimekuwa zikishuhudiwa katika mji wake wa nyumbani.
"Badala ya kushikiliwa na watoto wao, watoto hawa wako hospitali, wakinyonyeshwa na watu wasiowajua." anasema.
Kama daktari wa magonjwa ya akili, Firooza anataka kuchangia pakubwa katika kuhakikisha raia wengi wa Afghan wanapona majera na machungu ambayo wamekuwa wakikabiliana nayo.
'Ninafuraha kulelea mtoto'
Amewasiliana na baadhi ya rafiki zake kutafuta pesa za kununua nepi na maziwa ya unga, kwa ajili ya watoto hao wakati ambapo hawatakuwa tayari kunyonya.

Anasema, mbali na wale waliojeruhiwa, watoto wengine kwa sasa wanaruhusiwa kuondoka hospitali ya watoto ya Ataturk.
Lakini anawasiwasi kuhusu wale ambao hawana familia na kujiuliza wataenda wapi?
Kipaumbele itakuwa ni kwa watoto mayatima." Alisema, kwa uhakika.
"Nitakuwa mwenye furaha ikiwa nitaweza kuchukua mtoto na kumlea pamoja na kijana wangu."
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni