MLM Gateway - Helping network marketers build their business

Philip Mpango apendekezwa kuwa Makamu wa Rais Tanzania


Rais Samia Suluhu Hassan ampendekeza Philip Isdory Mpango kuwa makamo wa rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Jina hilo liliwasilishwa bungeni asubuhi ya Jumanne na mpambe wa rais katika bahasha maalum.Baada ya kupokea Spika Job Ndugai alilitangazia bunge hilo jina hilo lililopendekezwa na Rais Samia.Mara baada ya tangazo hilo bunge lililipuka kwa shangwe.Bwana Mpango amekuwa waziri mwandamizi katika serikali ya hayati John Magufuli akihudumu kama waziri wa fedha.Kwa sasa, bunge la Tanzania linatarajiwa kupiga kura ili kuthibitisha uteuzi huo wa Mpango.Na kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania, asilimia 50 ya wabunge wanatakiwa kuukubali uteuzi huo ili kuthibitishwa.

Kabla ya jina hilo kuwasilishwa bungeni hii leo, kwanza liliwasilishwa katika Kamati kuu ya chama tawala CCM na kuthibitishwa.

'Nimepigwa na butwaa'

Mara tu baada ya jina lake kusomwa Spika Ndugai alimpatia Mpango muda wa kujieleza ndani ya Bunge.

Mpango akaeleza kuwa hakujua chochote juu ya uteuzi huo na kwamba alipigwa na butwaa.

'...Hii ni heshima kubwa sana, sikuwahi kuota (kama nitaipata)...Mpaka Naibu Waziri wangu akiwa anajibu maswali asubuhi hapa, nilikuwa nafikiria majukumu yangu yanayonikabili ikiwemo mishahara ya wabunge ambayo baadhi imechelewa mpaka asubuhi hii. Nimepigwa na butwaa..."

Phillip Mpango ni nani?


Dkt.Mpango
Maelezo ya picha,Dkt. Phillip Mpango

Dkt. Philip Mpango amekua Waziri wa Fedha na Mipango katika Serikali ya Awamu ya Tano, ameteuliwa katika baraza la mwanzo la mawaziri la Rais John Magufuli.

Mwaka 2015 Alikua mbunge wa kuteuliwa.

Bwana Mpango ni mzaliwa wa Kigoma, baba yake ni marehemu Isidori Nzabhayanga Mpango, ambaye alizaliwa Kijiji cha Kasumo, Wilaya ya Kasulu.

Dkt. Mpango alizaliwa hapohapo Kasumo na ni kaka mdogo wa Askofu mstaafu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Tanganyika Magharibi - Kasulu mkoani Kigoma, Dk Gerard Mpango.

Dk Mpango ni mchumi mwenye shahada ya uzamivu ya uchumi.

Kuanzia miaka ya 1990 hadi 2000, alifanya kazi akiwa mhadhiri mwandamizi wa uchumi katika kitivo cha Biashara (sasa Shule ya Biashara) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Alikuwa akifundisha "Microeconomics", "Macroeconomics" (kwa mwaka wa pili) na "Public Finance" kwa mwaka wa tatu na kozi za uzamili. (Kwa tafsiri yangu, Uchumi mdogo, Uchumi mkubwa na masuala ya Fedha za umma.)

Amewahi kuwa Mchumi Mwandamizi wa Benki ya Dunia, Mkuu wa Kamati ya kumshauri Rais Jakaya Kikwete wakati huo kuhusu masuala ya uchumi, Katibu binafsi wa Rais anayeshughulikia masuala ya uchumi, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Uchumi, kabla ya kuhamishiwa Tume ya Mipango, Ofisi ya Rais.

Nyadhifa hizi zote amezishika wakati wa utawala wa Kikwete.

JPM alipoingia madarakani alimteua kuwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na baada ya siku chache akateuliwa kuwa Waziri wa Fedha na Mipango.

Katika uchaguzi wa mwaka 2020 alishinda kiti Cha ubunge jimbo la Buhingwe.

Kisha kuteuliwa tena kuwa waziri wa fedha na Mipango.


Share:

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

MAARUFU

ZA HIVI KARIBUNI